18 Aprili 2025 - 20:59
Source: IQNA
Hizbullah yaitaka OIC na Jumuiya ya Kiarabu Kutimiza Wajibu kwa Al-Aqsa

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu (Muqawama) ya Lebanon, Hizbullah, imetoa wito kwa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (AL), vituo vya kielimu na kisayansi vya Umma wa Kiislamu, pamoja na wapenda uhuru duniani kuchukua hatua za haraka kutimiza wajibu wao wa kihistoria kuhusu Msikiti wa Al-Aqsa katika mji wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na utawala haramu wa Israel.

Katika taarifa iliyotolewa Jumanne,  Hizbullah imelaani vikali uvamizi wa walowezi wa Kizayuni katika Msikiti wa Al-Aqsa na kufanya ibada za Kitalmudi humo kwa siku tatu mfululizo.

Hizbullah imesema kuwa lengo la uvamizi huo na udhalilishaji wa eneo hilo takatifu ni kuunda hali mpya na hatari ndani ya mradi wa ujenzi wa makazi na Uyahudi, kwa lengo la kubadilisha utambulisho wa Kiarabu na Kiislamu wa al-Quds na maeneo yake matakatifu.

Iliongeza kuwa utawala wa Kizayuni unaamini kimakosa kwamba uhalifu wake huko Gaza na Ukingo wa Magharibi utapotosha umakini wa umma kutoka kwa uvamizi unaoendelea dhidi ya Qibla cha kwanza cha Waislamu na moyo wa Palestina.

Utawala wa Kizayuni na walowezi wake wametumia fursa ya matukio ya kidini ya Kiyahudi kudhalilisha Msikiti wa Al-Aqsa, jambo ambalo limewakasirisha Waislamu kote duniani na kuchochea hisia za mataifa ya Kiarabu na Kiislamu, na kusisitiza haja ya kuchukua hatua madhubuti kukomesha mashambulizi hayo.

Harakati hiyo iliongeza kuwa, “Mataifa ya Kiarabu na Kiislamu yanao uelewa na mwamko wa kutosha kuinua sauti zao kwa kutumia njia zilizopo, kwani ukimya mbele ya mashambulizi na uhalifu huu unahamasisha adui wa Kizayuni kuendelea na mashambulizi yake huko al-Quds, Gaza, Ukingo wa Magharibi, Lebanon, Syria na Yemen na kuvuka mipaka ya tahadhari.”

Hizbullah ilitoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua madhubuti kusitisha uhalifu wa Kizayuni unaoungwa mkono na Marekani dhidi ya Palestina na eneo zima.

Mamia ya walowezi wa Kizayuni wamevamia eneo la Msikiti wa Al-Aqsa katika mji wa al-Quds Mashariki unaokaliwa kwa nguvu katika siku za hivi karibuni, sambamba na sikukuu ya Kiyahudi ya Pasaka.

Hatua hiyo imekumbana na lawama kali kutoka kwa maafisa wa Kipalestina na viongozi wa kidini, ambao wameielezea kama uchokozi wa makusudi.

Utawala wa Kizayuni umepeleka maelfu ya vikosi kuwalinda walozwezi wa Kizayuni wanaouvunjia heshima Msikiti wa Al-Aqsa.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha